YANGA
imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa
mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Al Hilal kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa,
Dar es Salaam. Swali kubwa lililoibuka baada ya matokeo hayo ni, tatizo
nini?
Mabao
ya Adama Coulibaly dakika ya 63 na Yasir Mozamil (dk 90) yaliitibulia
Yanga ambayo haikuwa imeruhusu idadi hiyo ya mabao tangu irejee katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita baada ya takriban
miaka 25.
Mabao
hayo yalitokana na safu ya beki ya Yanga chini ya mabeki wa kati,
Ibrahim Bacca na Dickson Job kutokuwa makini kuwazuia nyota wa Al
Hilal.
Pia
washambuliaji wa Yanga walishindwa kuwa na utulivu kwenye robo ya
mwisho ya uwanja kutokana na namna timu hiyo imekuwa ikijenga
mashambulizi.
Hata
hivyo, msimu huu Yanga ilianza vizuri michuano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika na hatua za awali hadi inafuzu makundi ilifunga mabao 17 bila ya
nyavu zake kutikiswa.
Novemba
15 mwaka huu, Yanga ilifanya mabadiliko ya benchi la ufundi ikimwondoa
Kocha Mkuu, Miguel Gamondi na msaidizi wake Moussa N’Daw, nafasi zao
zikachukuliwa na Sead Ramovic na Mustapha Kodro.
Leo ndiyo kilikuwa kibarua cha kwanza kwa makocha hao ambao wameanza kwa kichapo cha aibu kilichoibua maswali mengi.
Katika
dakika 45 za kwanza za mchezo huo wa Kundi A, Yanga ilionekana kuanza
kwa kasi huku Al Hilal ikiwa taratibu lakini kadri muda ulivyokuwa
unakwenda mambo yalikuwa yakibadilika.
Prince
Dube ambaye leo alikabidhiwa mechi hiyo maalum ikipewa jina lake,
alipata nafasi nyingi za kufunga lakini umakini mdogo ukaikosesha timu
yake mabao.
Dakika hizo 45 za kwanza, Dube alikosa nafasi tatu za wazi ambao kama angekuwa makini basi angeifungia timu yake.
Bado
kocha Ramovic atakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha wachezaji wake
wanashika falsafa zake akitaka kuona timu wanacheza soka la kasi lakini
mbele kwenye umaliziaji.
Washambuliaji
wa Yanga walishindwa kuwa na utulivu kwenye robo ya mwisho ya uwanja
kutokana na namna timu hiyo imekuwa ikijenga mashambulizi.
Kukosa
kwa nafasi hizo kumeendelea kuibua maswali ambapo Dube msimu huu
amekuwa hana wakati mzuri kitakwimu ukiachana na mabao matatu aliyofunga
hatua ya awali katika michuano hiyo, hana bao lingine.
Mbali
na Dube kukosa nafasi hizo, lakini kukosekana kwa Khalid Aucho eneo la
kiungo mkabaji imeonekana kuitesa zaidi Yanga na iliamua kumtumia
Mudathir Yahya aliyesaidiana na Duke Abuya.
Viungo
hao walionekana kushindwa kupandisha mashambulizi mbele na kuwaacha
viungo wa Al Hilal kutawala eneo hilo licha ya kwamba Yanga ndiyo
iliutawala mchezo kwa jumla kitakwimu za umiliki wa mpira.
Nguvu
kubwa waliyokuwa nayo Al Hilal ilikuwa kutumia pembeni kufanya
mashambulizi yake hasa upande wao wa kulia na Steven Ebuela alionekana
kumsumbua beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage.
Hata
bao la kwanza lililofungwa na Coulibaly alitumia udhaifu wa upande huo
wa Yanga, pia lile la pili lilipitia upande wa kulia wa Yanga.
Kwa
ujumla, wachezaji wa Yanga katika mchezo wa leo walicheza kwa morali ya
chini iliyowafanya kupoteza mchezo huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo
mbele ya Al Hilal.
Mara
ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 16, 2022 katika mchezo wa mtoano
wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa nchini Sudan na wenyeji Al Hilal
kushinda 1-0. Kabala ya hapo, Oktoba 8, 2022 jijini Dar es Salaam,
matokeo yalikuwa sare ya 1-1.
Ushindi
huo unamfanya Kocha Florent Ibenge wa Hilal kuendelea kufurahia
kukutana na Yanga kwani hajawahi kupoteza dhidi yao akishinda mara mbili
nyumbani na ugenini na kutoa sare mara moja katika mechi tatu
walizokutana.
Kocha
wa Al Hilal, Florent Ibenge amesema: “Yanga ni timu kubwa,
tulichokifanya ni kucheza kwa tahadhari, kipindi cha kwanza hakutuwa na
mikakati ya ushindi, lakini kipindi cha pili ndiyo tulihitaji ushindi.
“Mpango
huo ulikuwa ni kuhakikisha tunashambulia huku tukilinda lango letu kwa
tahadhari kubwa baada ya kuona kipindi cha kwanza wapinzani wameshindwa
kutufunga.”
Kocha
Ramovic amesema: “Inaumiza, nimeanza namatokeo mabaya ya kipigo, kama
timu kubwa tunarudi kujipanga na mechi zijazo, tunajua tuna mechi nyingi
mbele, tutahamikisha tunafanya vizuri.
“Ukiangalia
utimamu wa wachezaji upo chini kulinganisha na aina ya soka ninalotaka
kucheza ni vitu tofauti hivyo kuna kazi ya kufanya kuhakikisha mambo
yanakuwa mazuri.
“Huu
ni mwanzo, bado kuna mechi zingine za kucheza ambapo tuna wakati wa
kusahihisha makosa ambayo tumeona leo yametokea ikiwemo kushinda
kuzitumia vizuri nafasi tulizotengeneza.”
Licha
ya Yanga kupoteza mchezo huo, inaweza kurudi na kufanya vizuri baada ya
wapinzani wengine wa kundi lao, TP Mazembe na MC Alger kutoka 0-0 na
kufanya msimamo kusomeka hivi; Al Hilal pointi 3, MC Alger (1), TP
Mazembe (1) na Yanga (0).
Baada
ya mchezo wa leo, Novemba 30 mwaka huu Yanga itakuwa ugenini kucheza na
Namungo ukiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, kisha Desemba 6, itaenda
Algeria kupambana na MC Alger iliyofungiwa na Caf mashabiki wake
wasiingie uwanjani.